Jumatatu 19 Oktoba 2026 - 07:00
Mikusanyiko ya wananchi ni nguzo muhimu ya nguvu za kijeshi na kiusalama nchini Iran

Hawza/ Mkurugenzi wa Hawza nchini Iran, Ayatullah Alireza A‘rafi, amesema kuwa mikusanyiko ya wananchi ndiyo nguzo kuu inayoiimarisha nguvu za kijeshi na kiusalama za nchi, pamoja na kuwa kiungo kinachoiunganisha Iran na Mapinduzi ya Kiislamu na maoni ya umma duniani. Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuendeleza uwepo huo wa wananchi, kuimarisha ushiriki wa makundi mbalimbali ya jamii, kuongeza shughuli za misikiti na taasisi za utekelezaji wa serikali, na kugeuza uzoefu wa vita vya hivi karibuni vilivyolazimishwa dhidi ya Iran kuwa shule ya malezi na makuzi kwa kizazi cha vijana.

Kwa mujibu wa mwandishi wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Alireza A‘rafi aliyasema hayo alipokutana na baadhi ya wajumbe wa Baraza la Uratibu la Makao Makuu ya Mikutano ya Usiku ya Wananchi. Katika mkutano huo, alitoa shukrani kwa watu waliojitahidi katika miezi iliyopita, katika mazingira magumu zaidi ya nchi, kwa kusimamia na kuongoza ushiriki wa wananchi katika medani mbalimbali, alieleza kuwa harakati hiyo ni fahari kubwa.

Mkurugenzi wa Hawza nchini Iran, alikumbuka kwa heshima na taadhima manabii na mawalii wa Mwenyezi Mungu, mashahidi watukufu, na hususan Imam na Kiongozi aliyeuawa kishahidi. Alimuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu azidishe nusura na neema Zake kwa Umma wa Kiislamu, taifa la Iran, Mapinduzi ya Kiislamu, mhimili wa Muqawama, wananchi, vikosi vya ulinzi, uongozi, pamoja na watumishi wote wanaoshiriki katika harakati hii kubwa na mikusanyiko ya wananchi.

Vita Vitakatifu vya Miaka Nane: Uzoefu wa Kudumu katika Historia ya Iran na Dunia

Akiwa miongoni mwa mafaqihi wa Baraza la Walinzi wa Katiba, Ayatullah A‘rafi alizungumzia nafasi ya Vita Vitakatifu vya Ulinzi vya miaka minane katika mabadiliko ya Iran na eneo la Mashariki ya Kati. Alieleza kuwa uzoefu huo ni miongoni mwa vyanzo vikuu vya mabadiliko nchini Iran, huku akisema kuwa licha ya kupita miaka mingi tangu kumalizika vita hivyo, bado vinaendelea kuchambuliwa na kufanyiwa utafiti katika maeneo mbalimbali duniani. Aliongeza kuwa, kwa mitazamo mbalimbali, uzoefu huo ni tukio la kipekee katika historia ya siasa na mabadiliko ya kijamii.

Akikumbusha siku za mwisho za vita vya miaka minane vilivyolazimishwa dhidi ya Iran na kutolewa kwa tamko la Imam Khomeini (r.a.) kuhusu kukubaliwa kwa azimio la kusitisha vita, alisema: “Msisitizo wa Imam Khomeini (r.a.), katika tamko hilo na matamko yaliyofuata, kuhusu kuendelea kudumu Vita Vitakatifu vya Ulinzi kama mwenge wa uongofu, ni ukweli wa kihistoria. Nimeona katika sehemu mbalimbali duniani namna mataifa na wanafikra wanavyostaajabishwa na msimamo thabiti wa taifa la Iran katika kipindi chote cha miaka minane ya vita, licha ya matatizo na gharama zote zilizowakabili.”

Akifafanua zaidi, alisema kuwa: Vita Vitakatifu vya Ulinzi vinaendelea kuwa chanzo cha mabadiliko na msukumo duniani. Alisisitiza kuwa kusimama imara kwa taifa dhidi ya shinikizo na matatizo ya muda mrefu si uzoefu unaotoweka baada ya vita kumalizika, bali athari zake huendelea kuonekana katika vizazi vinavyofuata na katika uchambuzi wa kisiasa, kijeshi, kiutamaduni na kijamii.

Mashambulizi Dhidi ya Iran: Zaidi ya Tofauti za Juu Juu Miongoni mwa Mataifa Yenye Nguvu Duniani

Ayatullah A‘rafi alitoa tena pongezi kwa wananchi kwa kuchukua nafasi ya kuongoza na kusimamia mikusanyiko ya usiku huku akisisitiza: “Ninyi ni vinara wa sehemu ya Muqawama wa kina, mpana na wa kistaarabu wa taifa la Iran dhidi ya mashambulizi yasiyo na mfano katika historia ya zama za hivi karibuni, mashambulizi ambayo hayajawahi kushuhudiwa kabisa. Thamani ya kazi hii inadhihirika zaidi tunapozingatia vipimo vya makabiliano haya na ukubwa wa nguvu zinazoshiriki katika medani hii.”

Akizungumzia baadhi ya tofauti za kisiasa kati ya Wanademokrasia na Warepublikan nchini Marekani, pamoja na tofauti za mitazamo miongoni mwa nchi za Ulaya na vibaraka wao wasio na umuhimu mkubwa katika eneo hili, alisema kuwa haiwezekani kukana kuwepo baadhi ya tofauti za kimtazamo kati ya makundi na nchi hizo.

Hata hivyo, alieleza kuwa katika kiini cha sera kuu iliyobuniwa katika kipindi cha miaka miwili hadi mitatu iliyopita, kuna mwelekeo wa pamoja unaoonekana wazi, na kwamba wote wanakubaliana kuhusu jambo hilo. Alisisitiza kuwa huu ni ukweli unaopaswa kuzingatiwa wakati wa kuchambua hali ya dunia.

Mkurugenzi wa Hawza nchini Iran, akirejelea taarifa na jumbe zilizokuwa zikipokelewa katika wiki za mwanzo za vita, alisema: “Katika siku zilezile za mwanzo, tulikuwa tukipokea taarifa kutoka katika idara za kijasusi na pande mbalimbali, kuanzia Urusi hadi Pakistan na baadhi ya nchi nyingine, jumbe hizo zilikuwa na lugha iliyojaa huruma, huku baadhi ya pande zikishauri kutafutwa njia ya kumaliza hali hiyo, kwa sababu walidhani kuwa Iran isingeweza kabisa kuhimili mashambulizi haya hata kwa mwezi mmoja.”

Ayatullah A‘rafi aliendelea kusema kuwa; baadhi ya nchi hizo zilituma jumbe zilizowaeleza kuwa Wamarekani hawana huruma kabisa na kwamba Iran haikupaswa kuruhusu mambo kufikia hatua hiyo. Aliongeza kuwa baadhi ya jumbe hizo zilikuwa za dhati, huku nyingine zikiwa za juu juu tu. Hata hivyo, kwa ujumla, pande nyingi hazikutarajia kwamba Iran ingeweza kusimama imara dhidi ya shinikizo la aina hiyo katika wiki za mwanzo za vita. Baadhi yao walisema kuwa ikiwa kulikuwa na jambo lolote ambalo wangeweza kusaidia, walikuwa tayari kufanya hivyo, huku wengine wakisisitiza umuhimu wa kutafuta njia ya kumaliza hali hiyo.

Akieleza kuwa tathmini hizo zilionesha namna ambavyo wadau wengi wa kimataifa walivyokuwa wakitazama uwezo wa Iran wa kuhimili mashinikizo, alisema kuwa kile kilichotokea kwa vitendo kilikuwa tukio kubwa zaidi kuliko yale yaliyotangulia. Alifafanua kuwa tukio hilo linaendeleza mfululizo wa matukio ya kihistoria yaliyotokea huko nyuma, lakini linatofautiana nayo katika baadhi ya vipengele, kwa sababu katika hatua hii, mataifa makubwa yenye nguvu duniani yaliingia moja kwa moja katika medani.

Mkurugenzi wa Hawza nchini Iran, akizungumzia safari za wajumbe wa kisiasa na kidiplomasia kutoka nchi za eneo hilo, zikiwemo Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) na Saudi Arabia, alisisitiza kuwa diplomasia ina nafasi yake na inapaswa kutekeleza majukumu yake. Hata hivyo, alionya kuwa sambamba na harakati zinazoonekana kwa nje na tofauti zinazojitokeza katika misimamo ya nchi mbalimbali, ni muhimu pia kuzingatia malengo na hesabu zinazofanywa nyuma ya pazia.

Akieleza kuwa mabadilishano hayo ya maoni na mazungumzo ya kidiplomasia ni sehemu ya nje tu ya mambo, huku nyuma ya pazia pande zote zikikubaliana kwamba mazungumzo na fikra za Mapinduzi ya Kiislamu zinapaswa kudhoofishwa, aliongeza: “Katika uchambuzi wa hali hii, jambo kuu ni kutambua lengo linalofuatiliwa nyuma ya misimamo inayoonekana katika diplomasia. Lengo la pamoja ni kuishambulia fikra na mazungumzo ya Mapinduzi ya Kiislamu na kuvunja hadhi na utukufu wa taifa la Iran, ingawa huenda kukawa na tofauti kati ya wadau hao katika namna ya kulifuatilia lengo hilo.”

Ayatullah A‘rafi, huku akisisitiza kwamba haipaswi kuwepo hisia za utulivu wa kupindukia au kudhani kuwa vitisho vimekwisha katika hali ya sasa, alisema: “Kama ambavyo Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu pia alivyobainisha, licha ya mafanikio makubwa yaliyopatikana, bado kila mmoja anapaswa kuendelea kuwa katika medani na kutekeleza wajibu wake.

“Kazi iliyotekelezwa na taifa la Iran ni kubwa kiasi kwamba, Mungu apishe mbali, hata kama tutashindwa katika hatua hii, historia itaandika kuhusu taifa lililosimama imara kwa miaka miwili dhidi ya mawimbi makubwa zaidi ya kimataifa na mataifa yenye nguvu duniani, na likafanikiwa kujihifadhi. Hata hivyo, tunatumaini kwamba, kwa fadhila za Mwenyezi Mungu, jambo kama hilo halitatokea, na njia ya heshima na utukufu wa nchi itaendelea.”

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha